Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC) imetembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu mipya ya Chuo katika eneo la Banana, Dar es Salaam na kueleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika Oktoba 6, 2026, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri Bw. Juma Fimbo alipongeza maendeleo ya mradi na kusisitiza umuhimu wa kuendelea na kasi ya utekelezaji huku viwango vya ubora, usalama na mahitaji yaliyokusudiwa vikizingatiwa.
Kwa upande wake, Meneja Mradi Msaidizi Mhandisi Swalehe Nyenye alisema kuwa hadi kufikia Oktoba 6, 2026, utekelezaji wa mradi ulikuwa umefikia asilimia 29.18.
Aidha kwa upande wake Mkuu wa Chuo Bw. Aristid J. Kanje alisema Menejimenti ya CATC inaendelea kujiandaa katika nyanja za kitaaluma na kiutendaji ili kuhakikisha kuwa programu na huduma za mafunzo zitakazotolewa zinaendana na miundombinu mipya, mahitaji ya sekta na hadhi inayotarajiwa ya Chuo.
Mradi huo wenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 78 unahusisha ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya mafunzo ya usafiri wa anga. Kukamilika kwake kunatarajiwa kuongeza uwezo wa CATC katika kutoa mafunzo yenye viwango vya kimataifa na kuchangia katika kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha mafunzo ya usafiri wa anga barani Afrika na kwingineko.